Familia ya Morsi yasema 'ametekwa na jeshi'

Mwanawe wa kike aliyekuwa rais wa Misri na ambaye alipinduliwa na jeshi, Mohamed Morsi ametuhumu jeshi kwa kumteka babake.

Katika taarifa ya kwanza ya familia ya Morsi tangu kung'olewa kwake na jeshi mapema mwezi huu, Shaimaa Mohamed Morsi aliwaambia waandishi wa habari kuwa familia yake itamuhoji mkuu wa jeshi Generali Abdel Fattah al-Sisi, ikiwa chochote kitamtendekea babake.

Alisema kuwa familia yake itaiomba mahakama ya kimatifa ya uhalifu wa kivita kufanya uchunguzi katika kile alichokiita mapinduzi ya kijeshi yaliyosababisha mauaji na umwagikaji wa damu.

Mawakili wa Morsi walisema kuwa ni ukiukwaji wa haki zake za kibinadamu kwa kuwa anakamatwa bila makosa.