TZ yawaaga wanajeshi waliouawa Darfur

Rais wa Tanzania Jakaya kikwete sasa amelitaka taifa la Sudan kuanzisha uchunguzi ili kubaini ni nani aliyehusika na mauaji ya wanajeshi saba kutoka nchini humo.

Wanajeshi hao walifariki katika harakati za kulinda amani katika eneo la Darfur.

Saba hao wamepewa heshima za mwisho za kitaifa nchini Tanzania kabla ya kuzikwa manyumbani kwao.

Viongozi mbalimbali pamoja na raia walikusanyika katika viwanja vya wizara ya ulinzi na makao makuu ya jeshi Tanzania kutoa heshima hizo.

Miili ya wanajeshi hao iliwasili mjini Dar es Salaam siku ya Jumamosi, na kupokelewa na mamia ya waombolezaji walioongozwa na makamu wa rais Dokta Gharib Bilal, katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere kabla ya kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya kijeshi ya Lugalo.

Rais Kikwete aliwaongoza jamaa, familia na rafiki wa wanajeshi hao kuwapa heshima zao za mwisho kabla ya maziko nyumbani kwao.

Wanajeshi hao wa TPDF ni pamoja na Sajenti Shaibu Shehe, Corporal Oswald Chaulo, Corporal Mohammed Ally, Corporal Mohammed Chukilizo, Private Rodney Ndunguru, Private Fortunatus Msofe na Private Peter Werema.

Rais wa Sudan Omar Al Bashir wiki jana alimhakikishia rais Jakaya Kikwete kwa njia ya simu kuwa wote waliohusika katika kuwashambulia wanajeshi hao na kuwaua watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Rais Bashir alitoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo na Kikwete akiongeza kuwa anaamini waliohusika na mauaji hayo walikuwa wahalifu na kuwa lazima wasakwe.