10 wauawa kwenye mashambulizi Nigeria

Image caption Kuna hofu kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi huenda yakafanyika

Kumetokea msururu wa mashambulio katika eneo lenye idadi kubwa ya wakristu, mjini Kano, Kaskazini mwa Nigeria.

Ripoti zinasema kuwa watu kumi wamefariki na wengine kujeruhiwa.

Walioshuhudia mashambulizi hayo wanasema kuwa mabomu yalitegwa karibu na baa moja iliyokuwa na watu wengi,baadhi wakicheza mchezo wa Pool na table tennis.

Eneo hilo limewahi kulengwa na washambuliaji wa kundi la kiisilamu la Boko Haram.

Takriban watu 20 waliuawa katika eneo hilo mwezi Machi wakati basi moja lililokuwa na abiria kushambuliwa kwa bomu.

Polisi pia walisema kuwa watu kadhaa walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo yaliyofanyika Jumatatu jioni.

Mmoja wa walioshuhudia mashambilizi hayo aliambia shirika la habari la AP kuwa moja ya milipuko ilionekana kutoka katika gari moja aina ya Mercedes-Benz liliokuwa limeegeshwa karibu na duka moja liliokuwa linauza vileo na vinywaji vingine mbali mbali.

''Baada ya shambulizi la kwanza , nilijirusha katika bomba moja, kujificha. Kulikuwa na milipuko mitatu,'' alisema Kolade Ade aliyeshuhudia milipuko hiyo.

Eneo hilo limewahi kulengwa katika siku za nyuma na kundi la Boko Haram ambalo linapigana likitaka kuwa na utawala wa kiisilamu katika jimbo la Kano lililoko Kaskazini mwa nchi.

Kundi hilo ambalo jina lake linamaanisha ''elimu ya kimagharibi ni haramu'' limekuwa likilenga shule za umma kwa mashambulizi pamoja na kuwashambulia raia wa kawaida.

Tangu kundi hilo kuanza harakati zake mwaka 2009, zaidi ya watu 2,000 wameuawa.

Licha ya kuwa hakuna kundi lolote limedai kuhusika na mashambulizi yaliyotokea kwenye basi mjini Kano,mapema mwaka huu, kundi la Boko Haram lililaumiwa sana.

Wadadisi wanasema kuwa mji huo wenye idadi kubwa ya waisilamu una wasiwasi kuwa huenda kukatokea mashambulizi ya kulipiza kisasi, hasa kwani watu hujitokeza kwenye barabara sana wakati huu wa mfungo wa Ramadhan.