Wanariadha wa Kenya wakwama JKIA

Image caption Wanariadha wa Kenya

Kikosi cha wanariadha wa Kenya kinachoshiriki mashindano ya riadha ya dunia mjini Moscow Urusi, kimechelewa kuwasili mjini Moscow kutokana na upungufu wa mafuta katika uwanja rasmi wa ndege nchini humo.

Kikosi hicho chenye wanariadha 49 ni miongioni mwa masafiri 2,000 walioathirika kutokana na upungufu huo.

Afisaa mmoja katika uwanja huo alisema kuwa ndege 67 zilikatiza safari zao au kuzichelewesha baada ya kanieno kupungua kiasi cha kuathiri mtiririko wa mafuta.

Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ambao ni kitovu cha shughuli za usafiri wa ndege katika kanda ya Afrika Mashariki, ulifungwa kwa masaa hadhaa jana jioni.

Takriban abiria 1,000 walitafutiwa malazi katika hoteli mjini Nairobi.

Shughuli zimeweza kurejea kama kawaida katika uwanja huo na hivyo kikosi cha Kenya kuondoka Jumanne asubuhi.

Lakini msemaji wa shirikisho la riadha Kenya, Evans Bosire alisema kuwa kuchelewa kuwasili kwa wanariadha kutaathiri maandalizi ya kikosi hicho.

"sasa tuna siku mbili tu kujiandaa tukiwa huko kwa sababu mashindano yanaanza tarehe 10,'' alisema Bosire.

Kenya ilishinda medali saba za dhahabu katika mashindano hayo miaka miwili iliyopita mjini Daegu, Korea Kusini na kumaliza ya tatu.