''Hatuna imani na uchunguzi kuhusu Ponda''

Image caption Sheikh Isa Ponda

Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania umesema hauna imani na tume iliyoundwa na jeshi la polisi nchini humo kwa ajili ya kuchunguza tukio la kupigwa risasi kiongozi wa kidini Sheikh Ponda Issa Ponda.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Baruan Muhuza Mratibu wa mtandao huo Onesmo Ole Ngurumwa amewaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam leo kuwa jeshi hilo halina haki ya kujiundia tume ikiwa lenyewe ndiyo linatuhumiwa kumpiga risasi sheikh huyo.

Ngurumwa amesema kuwa inasikitisha kuona vyombo vya dola vinaendelea na uvunjaji wa sheria kwa kutumia nguvu inayokiuka haki za msingi za binadamu.

Msemaji wa Jeshi la polisi nchini humo Advera Senso ameiambia BBC mjini Dar es Salaam kuwa jeshi lake kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.

Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe, hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini.

Mapema Jumatatu asubuhi Baraza la waisilamu Tanzania-BAKWATA limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya taasisi za kisilamu na kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililosababisha kupigwa risasi kwa Katibu huyo wa Shura ya Maimamu nchini humo.

Kaimu Sheikh Mkuu wa Tanzania Alhad Mussa Salum amezungumza na waandishi wa habari Mjini Dar es Salaam na kusema kuwa japokuwa BAKWATA imekuwa ikipingana na misimamo ya Sheikh Ponda limesema serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata mkondo wa sheria.

Sheikh Ponda amekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na serikali ya Tanzania, anadaiwa kupigwa risasi baada ya kutokea vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr Jumamosi jioni.

Awali siku ya Jumapili Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu Tanzania, Alhajj Mussa Kundecha, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya nchi hiyo.

Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya Taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.

Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.

Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii