Duru ya pili ya uchaguzi Mali

Image caption Uchaguzi mkuu unatarajiwa kurejesha utulivu na uthabiti Mali

Watu nchini Mali walikwenda kwenye debe kupiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi mkuu mnamo Jumapili licha ya mvua kubwa kunyesha.

Uchaguzi huo unatarajiwa kurejesha utulivu na uthabiti nchini Mali baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vurugu.

Aliyekuwa waziri mkuu Ibrahim Boubacar Keita, aliyeshinda 40% ya kura kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi anakabiliana na Soumaila Cisse aliyekuwa waziri wa fedha.

Mwaka mmoja uliopita Mali imeshuhudia mapinuzi ya kijeshi pamoja na kusaidiwa na jeshi ya Ufaransa kupambana na waasi Kaskazini mwa nchi.

Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa sita jioni na matokeo yanatarajiwa kutolewa Ijumaa wiki hii.

Mshindi wa duru ya pili atasimamia msaada wa dola bilioni 4 ulioahidiwa na mataifa ya kigeni kuweza kuikarabati nchi.

Kikosi cha wanajeshi 12,600 cha Umoja wa Mataifa kinaanza kushika doria huku wanajeshi wa Ufaransa wakianza kujiandaa kuondoka.

Umoja wa Mataifa umesisitiza umuhimu wa uchaguzi huo katika kuijenga upya Mali pamoja na kuanza kwa mazungumzo ya kupatanisha watu wa nchi hiyo.

Baada ya kupiga kura mjini Bamako,Bwana Keita alisema kuwa watu walihofia kuwa idadi kubwa ya wapiga kura isingejitokeza kwenye duru ya pili.

Alisema matokeo yoyote yatakayotokana na uchaguzi huo, mshindi ni Mali.

Mpiga kura mmoja aliambia shirika la habari la AP kuwa bwana Keita alionyesha uzalendo wake na kuwa anatazamiwa na wengi kama mtu atakayeleta mabadiliko makubwa nchini humo.

Lakini mpiga kura mwingine Oumar Couilbaly, alisema mipango ya Cisse ni ya kina na inaweza kupatanisha watu wengi na ndio maana alimpigia kura.

Asilimia 49 ya wapiga kura milioni 6.8 waliojisajiwa walipiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo tarehe 28 mwezi Julai.

Bwana Cisse, aliyekuwa na kura nyingi kushinda wote katika duru ya kwanza ya uchaguzi alilalamika kuwepo visa vingi vya wizi wa kura huku kura laki nne zikisemekana kuharibika.

Hata hivyo, mahakama ya kikatiba ya Mali ilikataa madai hayo huku kiongozi wa waangalizi wa Muungano wa Ulaya akiusifu uchaguzi huo kwa ambavyo ulifanyika kwa uwazi.