Hali ya dharura yatangazwa Misri

Image caption Wafuasi wa Muslim Brotherhood

Vikosi vya usalama nchini Misri vimevamia kambi mbili za wafuasi wa rais aliyepinduliwa Mohammed Morsi mjini Cairo, kukiwa na taarifa za watu wengi kuuwawa.

Watu walioshuhudia wanasema wameona takriban maiti 40,lakini kundi la Ndugu wa Kiislamu Muslim Brotherhood linasema mamia ya watu wamekufa.

Tingatinga za kijeshi zilivamia kambi kuu nje ya msikiti wa mashariki wa Rabaa al-Adawiya.

Maafisa wa serikali wanasema kambi nyingine katika medani Nahda nayo pia ilivamiwa na wakaaji wake kutimuliwa.

Kuna taarifa za damu kumwagika kutoka kambi hizo huku waandishi Habari wakielezea waandamanaji wakipewa matibabu pembeni mwa maiti katika hospitali za dharura.

Binti wa umri wa miaka 17 wa mfuasi mashuhuri wa Muslim Brotherhood,Mohamed el-Beltagy ni miongoni mwa walioufa.

Asmaa al-Beltagy alipigwa risasi mgongoni na kifuani kwa mujibu wa kaka yake.

Mpiga picha wa shirika la Sky News, Mick Deane, nae pia ameuwawa katika ghasia hizo..

Kumekuweko pia na ripoti za ghasia katika maeneo mengine ya Misri.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali Mena linasema makanisa matatu yalishambuliwa katika mikoa ya kati ya Misri ,moja katika jiji la Sohag ambalo lina wakaazi wengi Wakristo wa madhehebu ya Kupti.

Shirika la habari la Reuters limearifu kutokea mapambano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa Morsi katika miji ya Assiut na Minya.

Wafuasi wa Morsi wanaarifiwa kufunga barabara katika mji wa kaskazini wa Alexandria.

Mamia ya wafuasi hao inaarifiwa wamekusanyika nje ya ofisi ya gavana mjini Aswan upande wa kusini.

Wizara ya mambo ya ndani imesema inaendelea na shughuli za kusafisha mitaa kandoni mwa Medani Nahda .

Wanaharakati wanamomuunga mkono Morsi walitimuliwa kutoka eneo la kuhifadhi wanyama na chuo kikuu cha Cairo kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Nile.

Idadi ya maafa bado haijulikani kwa uhakika na taarifa ni za kutatanisha.

Waandishi habari wa nchi za Magharibi wanasema wameshuhudia takriban maiti 40 katika eneo la msikiti wa Rabaa al-Adawiya.

Ikhwanonline, wavuti wa Muslim Brotherhood, unaowaunga mkono waandamanaji unasema zaidi ya watu 800 waliuwawa.

Wizara ya afya imetoa taarifa rasmi ikisema watu 95 wameuwawa.

Wizara ya mambo ya ndani imekanusha kuwa vifo hivyo vimetokana na vikosi kufyatua risasi za moto..

"vikosi vya usalama vilitumia gesi tu za kutoa machozi lkawatawanya waandamanaji ingawa vilishambuliwa kutoka ndani ya kambi hizo mbili,na kusababisha mauaji ya afisa mmoja na askari mmoja pamoja na polisi wanne kujeruhiwa na askari wawili" ilisema taarifa ya wizara hiyo.

Serikali imepongeza vikosi vya usalama kwa hatua yao ya kuwatimua watu waliokalia kambi hizo.