Misri: Waziri Mkuu atetea hatua ya polisi

Image caption Ni matokeo ya hatua ya polisi kutawanya wafuasi wa Mosri

Waziri Mkuu wa muda wa Misri Hazem Beblawi ametetea oparesheni kali iliyochukuliwa ya kuvunja maandamano ambayo yamekuwa yakifanywa na wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani , Mohamed Morsi.

Bwana Beblawi amesema walilazimika kuchukua hatua hiyo kwani kulikuwa na haja ya kujeresha hali ya usalama na utulivu nchini humo.

Hata hivyo waziri huyo mkuu amesema haukuwa uamuzi rahisi kuwatawanya wafuasi hao wa Morsi.

Serikali ambayo imetangaza hali ya hatari nchini humo imesema wakati wa oparesheni hiyo idadi ya watu waliofariki dunia ni 235

Lakini Msemaji wa Muslim Brotherhood, wamesema idadi ya watu waliouwawa ni zaidi ya 2,000 huku maelfu ya wengine wakijeruhiwa.

"Idadi ya waliofariki dunia ni karibu elfu mbili, na maelfu ya wengine wamejeruhiwa au kupotea . Haya yamekuwa ,mauaji ya kinyama,umekuwa ni umwagikaji wa damnu , tumekuwa na uchaguzi huru, tukawa na rais aliyechaguliwa kwa njia huru, tukawa na katiba iliyopigiwa kura kwa njia huru na bunge la juu la nchi, hayo yote yamepuuzwa na kwa wakati huu watu wanapigwa risasi kiholela. Demkorasia iko kichinjioni nchini Misri", amesema Ahmed Moustapha ,msemaji wa Muslim Brotherhood mjini London.

Nao waandishi wa habari mjini Cairo wameripoti kuona maiti nyingi. Hata hivyo imekuwa vigumu kujua idadi kamili ya waliouwawa.

Kwa wakati huu polisi wamewakamata wakuu kadhaa wa Muslim Brotherhood na pia wamechukuwa udhibiti wa kambi mbili ambazo zimekuwa zikitumiwa na waandamanaji.

Katika taarifa yake kupitia televisheni, Bwana Beblawi ameeleza masikitiko yake kwa mauji yaliotokea na kutoa hakikisho kuwa sheria ya hali ya hatari itaondolewa haraka iwezekanavyo.

Waziri huyo mkuu pia amesema kuwa polisi walikuwa wamepewa amri ya kutotumia silaha wakati wa kuwatawanya waandamanji.

Amri hiyo ya hali ya hatari inayotazamiwa kuwepo kwa mwezi mzima katika mji wa Cairo na katika mikoa megine itakuwepo kuanzia jioni saa Moja hadi kumi na mbili saa za Misri.