MDC Waondoa kesi yao Mahakamani.

Image caption Morgan Tsvangirai Kiongozi wa MDC

Chama cha MDC nchini Zimbabwe kimeondoa mashitaka yake dhidi ya ushindi wa Rais Robert Mugabe ikidai kwamba hawatatendewa haki.

Badala yake imewasilisha mashtaka tofauti ikidai maelezo kamili kutoka tume ya uchaguzi.

Lakini mahakama kuu imeahirisha uamuzi wake kwa kesi hiyo.

MDC inasema bila ya kupata maelezo kamili kama vile idadi ya watu waliopiga kura ambao hawakuorodheshwa katika daftari la wapigaji kura, hakitaweza kuthibitisha kwamba kulikua na wizi wa kura.

Madai ya MDC kuhusu wizi wa kura na unyanyasaji wa ZANU-PF yalipangwa kusikilizwa mnamo siku ya Jumaamosi.

"Naweza kuthibitisha tumeondoa mashtaka yetu dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Rais.

Kuna sababu kadhaa mkiwemo kushindwa kwa tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kutoa ushahidi muhimu katika swala hili" Amesema msemaji wa MDC Douglas Mwonzora.

Uamuzi huo unaondoa matumaini yoyote ya MDC ya kutumia mahakama, ambayo chama cha Tsvangirai kinasema yanadhibitiwa na ZANU-PF pamoja na taasisi nyingine za serikali katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika.

Mugabe, ambae ndie kiongozi mkongwe kupita wote barani Afrika ambae ametawala tangu uhuru kutoka Uingereza mnamo mwaka 1980,aliwaambia wakosoaji wake "wende wakajinyonge" na kuweka wazi kwamba hatavumilia lawama za nchi za Magharibi.

Serikali za nchi za Magharibi na hasa Marekani zimetaja mapungufu ya uchaguzi wa Julai 31 yaliyoelezwa na mashirika ya Zimbabwe,na kuhoji uhalali wa uchaguzi huo na zinazingatia kama waimarishe vikwazo dhidi ya Mugabe.

Lakini Mugabe hana wasiwasi akitiwa moyo na wachunguzi wa mataifa ya Afrika ambao walithibitisha uchaguzi huo kua huru kwa jumla uliooendeshwa kwa nidhamu na kuwahimiza wananchi wa Zimbabwe waendelee na maisha yao kwa amani..