EU yakemea mauaji yanayofanyika Misri

Image caption EU yaonya dhidi ya mauaji ya Misri

Muungano wa Ulaya umeonya Misri kuwa itarejelea uhusiano wake na nchi hiyo katika siku chache zijazo. Katika taarifa , Muungano huo umesema kuwa wito wa kuheshimiwa demokrasia na haki za kimsingi za binadamu haziwezi kuruhusiwa kuendelea kuvunjwa.

EU pia imeelezea wasiwasi wa kuongezeka umwagikaji wa damu. Umeongeza kuwa mauaji yaliyofanywa hayawezi kuelezewa wala kukubaliwa. EU imeahidi mabilioni ya dola kama mkopo na msaada kwa Misri kwa mwaka uliopita na mwaka ujao.

Mustakbal wa serikali

Baraza la mawaziri nchini Misri limeitisha mkutano wa dharura wakati ambapo mzozo wa kisiasa nchini humo kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Mohammed Morsi umesababisha raia wengi kupoteza maisha yao.

Kaimu waziri mkuu Hazem El Beblawi amependekeza kuvunjiliwa mbali kwa vuguvugu la Muslim Brotherhood ambalo bwana Morsi ni mwanachama .

Siku ya Jumamosi, polisi wakishirikiana na wanajeshi walifanikiwa kuwaondoa wafuasi wa vuguvugu hilo katika msikiti wa Al-Fateh mjini Cairo ambapo maelfu ya waandamanaji walikuwa wamekita kambi.

Vikosi vya usalama vimesema viliwakamata maelfu ya raia wakiwemo baadhi ya viongozi wa vugu vugu la Muslim Brotherhood na kwamba takriban watu 250 wanachunguzwa kwa mashtaka ya mauaji na ugaidi.