Maafisa 24 wa polisi wauawa Misri

Mpaka wa Rafa Sinai

Takriban maafisa 24 wa polisi kutoka Misri wameuawa kwenye shambulizi la kuvizia katika eneo la Rasi la Sinai. Duru zinaarifu polisi hao walikuwa kwenye msafara wa mabasi mawili yaliyoshambuliwa na kundi la watu waliokua na silaha karibu na mji wa Rafa mpaka na Ukanda na Gaza.

Polisi watatu walijeruhiwa kwenye shambulio hilo. Katika siku za karibuni jeshi la Misri limeimarisha operesheni dhidi ya wanamgambo eneo la Sinai hususan baada ya mashambulizi kuongezeka tangu kuanguka kwa uliokua utawala wa Hosni Mubarak mwaka 2011.

Misri imekua ikishika doria eneo la Sinai chini ya mkataba wa mwaka 1979 kati ya Israel na Misri.Mashirika ya habari yanaripoti kwamba wanaume wanne waliojihami kwa silaha walisimamisha mabasi hayo na kuwaamrisha abiria wote kuondoka kisha wakaanza kuwapiga risasi.

Baadhi ya duru zinasema washambuliaji hao walitumia maroketi kulenga mabasi hayo. Utawala wa mpito umetangaza hali ya hatari kufuatia maandamano ya umma yaliofuatia kuondolewa mamlakani kwa Muhammed Morsi kama Rais wa nchi hiyo. Amri ya kutotoka nje usiku imewekwa mji mkuu Cairo.

Zaidi ya watu 800 wakiwemo polisi 70 wameuawa tangu Jumatano ya wiki jana wakati jeshi lilipovunja kambi za wafuasi wa vuguvugu la Muslim Brotherhood anakotokea Morsi. Na hapo Jumapili mahabusu 36 walikufa wakati wakisafirishwa katika jela moja nje ya mji wa Cairo.Serikali na jeshi wamesema mahabusu hao walikosa hewa kwenye gari walimokua. Hata hivyo Muslim Brotherhood wametaja kitendo hicho kama mauaji ya kinyama.

Huku haya yakiarifiwa Muungano wa Ulaya umeitisha kikao cha dharura kujadili uhusiano wake na Misri. Muungano huo umetoa taarifa ya pamoja na kusisitiza haja ya kumaliza ghasia mara moja.Wafuasi wa Morsi wametaja kuondolewa kwake kama mapinduzi, lakini jeshi na serikali zinasema vuguvugu la Muslim Brotherhood liliendesha kampeini ya ugaidi tangu kuondolewa kwa kiongozi wake kama Rais.