Brotherhood yalaani kukamatwa kwa Badie

Mohammed Badie
Image caption Kiongozi wa Muslim Brotherhood yuko kizuizini huku akikabiliwa na tuhuma za kuchochea ghasia na mauaji

Vugu vugu la Muslim Brotherhood limelaani kukamatwa kwa kiongozi wake Mkuu Mohammed Badie, kwa tuhuma za kuchochea ghasia na mauaji.

Msemaji wa kundi hilo amesema kukamatwa kwa kiongozi huyo ni njama ya kulipiza kisasi mapinduzi ya umma yaliyomuondoa madarakani Rais wa zamani Hosni Mubarak mwaka wa 2011. Badie alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka makaazi yake karibu na kitovu cha maandamano ya wafuasi wa Brotherhood Mjini Cairo.

Jeshi la Misri lilivunja kambi hizo wiki jana ambapo kulitokea maafa ya raia wengi. Wakati huo huo Aliyekua Makamu wa Rais Mohamed ElBaradei anakabiliwa na mashtaka ya kusaliti imani ya taifa.

Bw ElBaradei aliondoka nchini Misri baada ya kujiuzulu kufuatia hatua ya jeshi kuvunja kambi za wapinzani na kusababisha maafa ya mamia ya watu.Utawala wa mpito umetangaza hali ya hatari nchini Misri na kumekua na operesheni kali dhidi ya wafuasi wa Rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi.

Hapo Jumanne Vugu vugu la Muslim Brotherhood limewaomba wafuasi wao kuendelea na maandamano kushinikiza jeshi imrejeshe madarakani Bw. Morsi. Kwenye mkutano na waandishi wa habari mmoja wa viongozi wa chama cha Justice And Freedom Party, mrengo wa kisiasa wa Brotherhood alisema kukamatwa kwa kiongozi wake hakutadidimiza harakati zao.

Naibu kiongozi wa vugu vugu hilo Mahmoud Ezzat ametangazwa kama kaimu kiongozi. Mohammed Badie amekua akiongoza maandamano ya wafuasi wa Bw Morsi. Hata hivyo aliingia mafichoni baada ya serikali kutangaza onyo la kuvunja kambi za waandamanaji.

Kiongozi huyo anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ghasia na mauaji ya raia wanane waliopinga Muslim Brotherhood. Mzozo wa kisiasa nchini Misri umepelekea mauaji ya watu 900 na maelfu kujeruhiwa.

Mauaji hayo yamepelekea laana za kimataifa, baadhi ya wafadhili wakitarajiwa kukutana Jumatano kuamua ikiwa watasitisha msaada kwa utawala wa Misri.

Wakati huo huo Misri imetangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kufuatia mauaji ya maafisa 24 wa polisi katika Rasi ya Sinai. Wanamgambo wa kiisilamu wamelaumiwa kwa kutekeleza mauaji hayo.