Vifo vya Goma vyachunguzwa

Mtu aliyekufa katika shambulio la mizinga akibebwa na kundi la watu Goma

Kikosi cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo kimeanzisha uchunguzi kuhusu vifo vya waandamanaji wawili mjini Goma.

Walioshuhudia tukio hilo waliliambia shirika la habari la Ufaransa kwamba watu hao walikufa wakati waandamanaji walipojaribu kuvamia kambi ya kikosi hicho karibu na uwanja wa ndege.

Waliwatuhumu askari wa Umoja wa Mataifa kutoka Uruguay kuwa walifyatua risasi dhidi ya waandamanaji.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa, MONUSCO, bado kujibu tuhuma hizo.

Mamia ya watu waliandamana hapo jana kupinga mapigano yanayoendelea baina ya MONUSCO na wapiganaji wa M23.

Na watu kama watatu piya walikufa jana pale eneo la makaazi lilipopigwa na mizinga - Umoja wa Mataifa unawalaumu wapiganaji kwa hayo.

Lakini kundi la M23 limesema kamwe halikushambulia mji wa Goma.

Kiongozi wa kundi hilo, Betrard Bisimwa akizungumza na BBC amesema kuwa hivyo ni visingizio vya kutaka jeshi la Umoja wa Mataifa kuingilia kati.