Raia wakimbia makwao C.A.R

Image caption Wapiganaji wa Seleka katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati

Maelfu ya raia wametorokea katika uwanja mkuu wa ndege wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati ili kuepuka ghasia na machafuko.

Raia hao walipiga kambi kwa muda katika barabara kuu ya ndege na kuzuia ndege kadhaa kutua katika uwanja huo.

Walioshuhudia wanasema wakaazi wa wilaya moja karibu na uwanja huo, walianza kukimbia makwao baada ya wapiganaji wa kundi la waasi wa Seleka kuanza kufyatua risasi katika eneo hilo.

Jamuhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na machafuko tangu waasi walipomuondoa madarakani rais Francois Bozize.

Siku ya Jumapili, rais wa Ufaransa, Francois Hollande, alitoa wito kwa baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa, kurejesha hali hali ya utulivu nchini humo, akionya kuwa hali inaweza kugeuka na kuwa kama ilivyo nchini Somalia.