Mzozo wa Syria wachukua mkondo mpya

Image caption Shule iliyoshambuliwa Syria

Serikali ya Marekani imesema, itakabiliana na mzozo wa Syria kwa njia ambayo itakuwa na manufaa kwa maslahi yake, baada ya wabunge wa Uingereza kupinga jeshi la nchi hiyo kuhusika moja kwa moja na mzozo huo.

Lakini Marekani imesema kuwa nchi ambazo zinakiuka sheria za kimataifa kuhusu utumiaji wa silaha za kemikali, ni sharti ziwajibishwe.

Utawala wa Washington, umeishutumu jeshi la serikali ya rais Bashar al Assad kwa kutumia silaha za kemikali, madai ambayo yamepingwa vikali na utawala wa Damascus.

Uamuzi huo wa wabunge wa Uingereza, unamaanisha kuwa Uingereza haitahusika kwa vyovyote vile katika mashambulio ya kijeshi dhidi ya Syria, yatakayoongozwa na Marekani.

Licha ya uamuzi huo wa Uingereza, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, amesema serikali ya nchi hiyo itaendelea kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa jamii ya kimataifa, ili kuchukua hatua ya pamoja kujaribu kutatua mzozo huo wa Syria.

Silaha za sumu zilituma-Marekani

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ikulu ya White Houe, rais Obama atachukua uamuzi ambao utakuwa na manufaa kwa maslahi ya Marekani.

Image caption Waziri wa mambo ya nje wa Marekani

Taarifa hiyo imenadi kuwa rais Obama, anaamini kuwa kuna haja ya Marekani kuingilia kati mzozo huo.

Na katika kikao cha maafisa wakuu wa idara ya ujasusi na wabunge wa Congress, kujadili uwezekano wa kuanzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya wanajeshi wa rais Assad, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, amesema utawala wa Washington hautalemazwa au kuhujumiwa na sera za kigeni za mataifa mengine.

Mwanachama mmoja wa kamati ya masuala ya nchi za kigeni, Eliot Engel wa chama tawala cha Democratic nchini Marekani, amewaambia waandishi wa habari kuwa utawala wa rais Obama, unaamini kuwa silaha za kemikali zilitumika kimakusudi na utawala wa rais Assad.

Engel amesema wamepata ushahidi ikiwa ni pamoja na mawasiliano kutoka kwa maafisa wakuu wa serikali ya Syria.

Watu mia tatu hamsini na watano wameripotiwa kuuawa kufuatia shambulio hilo la kemikali katika eneo la Ghouta,viungani mwa mji mkuu wa Damascus tarehe 21 mwezi huu.