Wachunguzi wa silaha waondoka Syria

Mchunguzi wa Umoja wa Mataifa akipekua eneo linalosemekana silaha za kemikali zilitumika nchini Syria

Wachunguzi wa silaha za kemikali wa Umoja wa Mataifa wameondoka Syria baada ya kuchunguza madai ya utumizi wa silaha za sumu katika kitongoji cha Damascus juma lilopita, ambao inasemekana uliuwa watu zaidi ya 1,400.

Maafisa hao wameondoka saa kadha baada ya serikali ya Marekani kueleza sababu za kupanga kuishambulia serikali ya Syria.

Rais Obama amesisitiza kuwa bado hakuamua aina ya hatua ya kijeshi atayochukua.

Wakaguzi wa silaha wanatarajiwa kukabidhi ripoti yao kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban-Ki Moon, katika majuma mawili yjayo, baada ya kukagua sampuli walizobeba kutoka Syria kwenye maabara - sampuli za udongo, damu na mikojo.