Wachimba migodi waanza mgomo A.Kusini

Image caption Mgomo huu unatishia kuathiri sekta ya madini nchini Afrika Kusini

Takriban wachimba migodi 80,000 wa dhahabu nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kuanza mgomo kudai nyongeza ya mishahara.

Chama cha kitaifa cha wafanyakazi wa migodini kinataka waongezwe mishahara kwa asilimia sitini.

Wafanyakazi hao wiki jana walikataa pendekezo walilopewa la nyongeza ya asilimia 6 ambacho ni kiwango cha mfumuko wa bei kwa sasa.

Sekta ya madini ya dhahabu ndio moja ya sekta kubwa duniani lakini imekuwa ikikumbwa na misukosuko katika miaka ya hivi karibuni huku ile ya madini ya platinum ikijikwamua kutokana na athari za migomo iliyokumba sekta hiyo mwaka jana.

Inakisiwa kuwa migomo hiyo ya wachimbaji migodi ikiwa itafanyika, itapotezea nchi hiyo zaidi ya dola milioni 30 kila siku.

Wamiliki wa migodi wanaonya kuwa migomo hiyo huenda ikasababisha migodi ya dhahabu kufungwa na maelfu kupoteza kazi zao kufuatia kushuka kwa bei ya dhahabu.

Wanasema kuwa gharama za uchimbaji dhahabu zimepanda kwani wamelazimika kutumia pesa nyingi zaidi katika shughuli nzima za uzalishaji.

Kwa miezi mingi Afrika Kusini ilikuwa nchi yenye kuzalisha zaidi dhahabu ikiwa inazalisha asilimia 68 ya dhahabu yote duniani katika miaka ya sabini.

Lakini kwa sasa iko katika nafasi ya tano katika uzalishaji wa madini hayo ikiwa ni asilimia sita pekee ya dhahabu yote duniani ingawa bado ni sekta muhimu sana katika uchumi wa nchi hiyo.

Rais Jocob Zuma ametaka pande zote mbili kwenye mgogoro huu kuafikiana ili kuzuia hasara kwa pande zote mbili.

Wafanyakazi watalazimika kuondoka kazini saa sita asubuhi kwa mujibu wa msemaji wa chama cha wafanyakazi hao, alisema Lesiba Seshoka.

Hata hivyo alikanusha madai kuwa nyongeza wanayotaka ya asilimia 60 ni kubwa sana. Chama cha wafanyakazi cha NUM kinawakilisha asilimia 64 ya wafanyakazi 120,000 wanaochimba dhabahu migodini.

Wananchi wa Afrika Kusini walishangazwa sana mwaka jana wakati polisi walipowaua wachimba migodi 34 wa Platinum waliokuwa wamefanya mgomo haramu uliokuwa umeitishwa na chama chao na kutuhumu NUM kuwa na uhusiano wa karibu na serikali.

Mwandishi wa BBC Mike Wooldridge mjini in Johannesburg anasema kuwa huku uchaguzi ukisubiriwa mwaka ujao, serikali inatumai kuwa itaweza kukabili migomo hiyo, katika msimu huu ambapo watu wengi wanaomba nyongeza ya mishahara.