TB ilitokana na wanadamu sio wanyama

Image caption Vimelea vya TB

Kikundi cha wanasayansi wa kimataifa kinasema kuwa homa ya mapafu ilitokana na waafrika waliokuwa wana hama hama miaka 70,000 iliyopita

Utafiti wa wanasayansi hao bila shaka ni kinyume na dhana kwamba homa ya Mapafu ilitokana na wanyama miaka 10,000 iliyopita na kusambaa hadi kwa binadamu.

Utafiti huo unaonyesha uhusiano mkubwa ulioko kati ya historia ya binadamu na homa ya mapafu au TB.

Ugonjwa huo husababisha zaidi ya vifo milioni moja kila mwaka.

Utafiti wa awali ulionyesha kuwa homa ya mapafu ambayo huwaathiri wanadamu ilianza kusikika tu miaka 10,000 iliyopita wakati idadi ya watu ilipoanza kuongezeka huku wengi wakianza kufanya kilimo.

Watafiti walikusanya taarifa za kijiografia na data kuhusu genetiki za watu kutoka kwa aina 259 ya vimelea vya homa ya TB kwa lengo la kufananisha na historia ya binadamu Afrika.

Profesa Sebastian Gagneux, kutoka katika taasisi ya magonjwa ya kiafrika nchini Uswizi alisema kuwa , walichogundua ni kuwa binadamu wa kwanza alitokea Afrika sawa na maambukizi ya kwanza ya Kifua Kikuu kuripotiwa miaka 60,000 iliyopita , ikisemekana kuwa mapema mno ikilinganishwa na ilivyodhaniwa.

''Lengo letu ni kutaka kuthibitisha kuwa ugonjwa wa kifua kikuu ulianza kuenea miongoni mwa binadamu na baadaye kuenea kwa wanyama,'' alisema Profesa Sebastaian.

Swali sasa ambalo wanasayansi wanahoji ni vipi vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu viliweza kudumu kwa miaka 60,000 miongoni mwa watu wachache sana.

Moja ya mambo yanayowashangaza wanasayansi ni kuwa mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa miaka mingi kabla ya kuanza kuonyesha dalili za kuambukizwa.

Hali ya ugonjwa huo kukaa kwa miaka mingi bila ya kuonyesha dalili ndiyo inawafanya watafiti kuamini kuwa sababu kuu ya ugonjwa kudumu kwa muda huo mrefu.

Wakati idadi ya watu ilipoanza kuongezeka ugonjwa huo nao ukaanza kusambaa.

Na wakati watu walipoendelea kuongezeka ndiposa ugonjwa huo nao ulipoendelea kuenea.

Hatua itakayofuata katika utafiti wa wanasayansi hawa ni kutumia data ya jenetiki kuelewa ambavyo vimelea vya TB viliweza kudumaa kwa miaka mingi kabla ya kujitokeza kama ugonjwa mwilini mwa mtu.

Ugonjwa wa Kifua Kikuu ni tisho kubwa duniani kwa kusababisha vifo milioni 1.4 mnamo mwaka 2011, kulingana na shirika la afya duniani.

Ikiwa wanasayansi wanaweza kuelewa uhusiano uliokuwepo kati ya ugonjwa wa TB wanadamu,inaweza kusaidia katika juhudi za kupunguza maambukizi yake.