Waziri wa serikali anusurika kifo Misri

Image caption Waziri Mohammed Ibrahim

Waziri wa mambo ya ndani nchini Misri, amenusurika jaribio la kumuua nje ya nyumba yake mjini Cairo.

Maafisa wanasema kuwa mlipuko ulisikika na kwamba ulikuwa unamlenga waziri huyo Mohammed Ibrahim. Hata hivyo inasemekana kuwa hakujeruhiwa hata kidogo.

Kuna taarifa za kutofautiana kuhusu ikiwa lilikuwa shambulizi la bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari au kilipuzi kilichorushwa kutoka ndani ya jengo lililoko mjini Nasr.

Watu kadhaa wanasemekana kujeruhiwa.

Aidha maafisa wanasema kuwa polisi wamewaua washambuliaji wawili.

Hili ni shambulizi la kwanza lililolenga afisaa wa ngazi ya juu, huku nchi hiyo ikisalia katika hali ya taharuki kutokana na malumbano kati ya serikali ya kijeshi na chama cha Muslim Brotherhood.