Visa vya Malaria vyaongezeka Chad

Image caption Mwanawe Halima, Salimata anatibiwa Malaria

Mpango wa dharura unaendelea katika eneo la Salamat nchini Chad baada ya ongezekao la visa vya maambukizi ya Malaria kuripotiwa.

Shirika la madaktari wasio na mipaka, (MSF) linasema kuwa idadi ya visa vya maambukzi mapya ilipanda kutoka 1,228 katika wiki ya kwanza ya mwezi Agosti hadi 14,021 mwishoni mwa mwezi.

Visa vya maambukizi ya Malaria, hupanda wakati wa mwezi Julai hadi Novemba wakati wa msimu wa mvua.

Lakini washauri wa afya wa MSF nchini Chad, Daktari Turid Piening, amesema ongezeko kubwa la visa vya Malaria wakati huu sio jambo la kawaida.

Alisema zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaotafuta matibabu , wanakuja kwa sababu wameambukizwa Malaria.Kawaida walioambukizwa wakati huu huwa kati ya asilimia 30 hadi 40

Ugonjwa wa Malaria ndio unaogunduliwa sana kuwa tatizo kwa wagonjwa katika vituo vya afya nchini humo.

Nusu ya vifo vyote vinavyoripotiwa nchini Chad vinatokana na Malaria, na watoto wengi pia wanafariki kutokana na ugonjwa huo kulingana na MSF.

Takwimu zilizotolewa na shirika la afya duniani hivi karibuni, zinaonyesha kuwa zaidi ya watu laki sita walifariki kutokana na Malaria duniani mwaka 2010, wengi wao wakiwa watoto barani Afrika.

Kikundi cha wataalamu wa MSF wanaofanya kazi katika mji wa Am Timan walifahamishwa na maafisa wa afya wa serikali kuhusu ongezeko la visa vya Malaria, mnamo mwezi Julai

Hata hivyo, ongezeko hili halitajwi kuwa mlipuko wa ugonjwa huo.

''Watu wengi waliamza kugonjeka kijijini kwetu , wakawa wanatetemeka na kuonekana kama wasio katika hali ya kawaida,'' alisema Halima Ibrahim ambaye mtoto wake mwenye umri wa miaka minane alishikwa na Malaria.

"mwanangu alianza kutetemeka, pia alikuwa analalamika kuhusu kuumwa na kichwa huku akihisi uchungu kwenye viungo vyake. Tuliomba lakini alisalia tu kuwa mgonjwa.''

Daktari Piening alisema kuwa licha ya Malaria kuwa ugonjwa unaoua watu wengi mjini Salamat , watu wa eneo hilo hawana uwezo wa kupata madawa muhimu ya kuokoa maisha yao wala vyandarua.

"wengi wao ni watu wa kuhama hama. Njia bora zaidi ya kujilinda kutokana na Malaria, ni kujifunika kwa vyandarua ambavyo vinaweza kuzuia maambukizi kwa asilimia 60.

Hata hivyo haijulikani sababu kubwa ya kuongezeka kwa visa vya Malaria katika eneo la Salamat