Kenya na Nigeria kushirikiana kibiashara

Image caption Ziara ya Godluck ni ya kwanza rasmi nchini Kenya

Kenya na Nigeria zimetia saini mkataba utakaoimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Katika taarifa ya pamoja , Rais Kenyatta na mwenzake wa Nigeria Goodluck Jonathan pia walikubaliana kufanya kazi pamoja katika sekta ya kilimo na uvuvi na mifugo.

Serikali hizo mbili zimesaini makubaliano ya pamoja kuhusu uhamiaji ambapo huenda visa zikaondolewa kwa wanigeria na wakenya , swala la uhalifu, biashara haramu ya mihadarati na kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Nchi hizo pia zimekubaliana kupambana dhidi ya makundi ya ugaidi kama vile Al-Shabab na Boko Haram katika maeneo yao.

Rais Kenyatta pia alikubali kufanya ziara ramsi nchini Nigeria katika siku za baadaye.

Alisema kuwa nchi hizo mbili zitaimarisha biashara na uekezaji kwa kubuni mazingira bora ya utalii na utamaduni.

Vile vile Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ametoa wito kwa dunia kusaidia Wakenya kuimarisha demokrasia na utawala bora badala ya kujivuta kwa mambo yaliyopita ambayo Wakenya wanataka kusahau.

Amesema kwamba uchaguzi wa March ulidhihirisha kuwa waKenya wana uwezo wa kusuluhisha matatizo yao.

Kiongozi wa Nigeria aliyasema hayo katika bunge la Kenya,siku moja baada wabunge kupitisha hoja ya kutaka nchi hiyo ijiondoe kutoka mahakama ya ICC.