Ghana yapinga mafuta yaliwaua Nyangumi

Image caption Zaidi ya Nyangumi 15 wamefariki tangu mwaka 2009

Ghana imepuuzilia mbali madai kuwa shughuli za kuchimba mafuta kwenye ufuo wake zimesababisha vifo vya Nyangumi wawili wiki moja iliyopita.

Kikundi kimoja cha wanaharakati wa mazingira kimesema kuwa Nyangumi hao, walianza kuonekana tangu shughuli za uzalishaji mafuta zilipoanza mwaka 2009.

Wanaharakati hao wanapendekeza kuitishwa kwa jopomaalum kuchunguza vifo hivyo.

Kampuni hizo za mafuta, zilikataa kuzungumzia madai hayo lakini shirika la kulinda mazingira lilisema kuwa hapakuwa na uhusiano wowote kati ya sekta ya mafuta na Nyangumi hao waliofariki.

Hata hivyo liligundua kuwa matukio kama haya huripotiwa kote duniani na wala sio Ghana pekee.

Shirika hilo limesema hakuna misingi ya kutosha kusema kuwa Nyangumi na wanyama wengine wa bahari waliofariki hupatikana tu katika sehemu ambako shughuli ya uchimbaji wa mafuta hufanyika.

Liliongeza kuwa haijulikani kilichosababisha vifo vya Nyangumi hao, hali ambayo bila shaka inaleta wasiwasi mkubwa kwa shirika hilo.

Wakereketwa wa mazingira leo wamechapisha taarifa kwenye mitandao ya Ghana wakitoa kauli mbiu ya kutaka kuokolewa kwa Nyangumi wao.

Taarifa hiyo ilisema kuwa ''Ingawa vifo vya Nyangumi hao ni jambo la kawaida, idadi ya vifo vilivyotokea katika miaka minne iliyopita, inaleta wasiwasi.''

Inasema kuwa Nyangumi watano waliokuwa wamekufa walipatikana ufiuoni wiki jana na kufikisha idadi ya Nyangumi waliofariki ufuoni tangu mwaka 2009 kuwa 16.