'Vikosi vya usalama' vilimteka bintiye Senussi

Image caption Senussi alikuwa mshirika mkubwa sana wa hayati Muamar Gaddafi

Kundi la wapiganaji linalohusishwa na wizara ya mambo ya ndani nchini Libya limesema kuwa ndilo limemteka mwanawe wa kike aliyekuwa mkuu wa ujasusi nchini Libya Abdullah al-Senussi kwa usalama wake mwenyewe.

Anoud Abdullah al-Senussi alitekwa nyara alipokuwa anaondoka kutoka gerezani mjini Tripoli siku ya Jumatatu baada ya kuhudumia kifungo chake cha miezi kumi baada ya kupatikana na hatia ya kutumia pasi bandia ya usafiri.

Mtu mmoja kutoka kabila lake anasema kuwa yuko katika hali nzuri.

Bwana Senussi yuko gerezani kwa kile kinachosemekana kuwa kuhusika kwake katika uhalifu wakati wa uliokuwa utawala wa Muammar Gaddafi.

Pia anatakikana na mahakama ya kimataifa ya (ICC), ambayo imemtuhumu kwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa mapinduzi ya kumuondoa mamlakani Gaddafi mwaka 2011.

Taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Facebook wa kundi lililomteka Bi Senussi inasema kuwa walifanya hivyo ili kumlinda kutokana na kutekwa nyara na kundi hasimu.

Kundi hilo la FSRU liko chini ya kamati ya usalama iliyoundwa na wizara ya mambo ya ndani na linajumuisha wapiganaji waliochukua silaha kumuondoa mamlakani Gaddafi.

Mwandishi wa BBC, Rana Jawad mjini Tripoli anasema kuwa serikali imekuwa na wakati mgumu kuvunja kundi hilo.

Bi Senussi alifanikiwa kuzungumza na mamake, Abdelgader Ibn Gassim.

"tuna matumaini kuwa ataachiliwa katika muda wa siku mbili. Yuko mjini Tripoli katika moja ya makao makuu ya usalama.''

Mnamo Jumatatu , waziri wa sheria, Salah al-Marghani alisema kuwa watu waliokuwa wamejihami waliwafyatulia risasi polisi waliokuwa wanamsindikiza Bi Senussi kutoka katika jela la al-Rayoumi kabla ya kumetaka nyara.