Cameroon yailaza Libya bao 1-0

Image caption Timu ya soka ya Cameroon

Cameroon imejipatia nafasi ya kushiriki michuano ya mwisho ya kufuzu michuano ya kombe la Dunia kwa nchi za Afrika mwaka 2014 nchini Brazil.

Indomitable Lions waliicharaza Libya bao moja bila kwenye mechi ambayo ilichezwa mjini Yaounde Jumapili.

Cameroon walijitosa uwanjani wakijua fika kuwa hata ikiwa wangeenda Sare na Libya matokeo hayo hayangeathiri nafasi yao kushiriki, na haya yote ni kutokana na timu ya Togo kutumia mchezaji aliyeharamishwa Alexis Romao kucheza wakati wa mechi yao na Cameroon mnamo mwezi Juni.

Hali hii ilisababisha kufutiliwa mbali kwa matokeo ya mechi hiyo.

Mchezaji Aurelien Chedjou ndiye aliyefunga bao la ushindi wakati wa kipindi cha kwanza cha mechi hiyo.

Chedjou alifunga bao lake kunako dakika tatu kabla ya kipindi cha mapumziko na ushindi bila shaka ukawa wa Cameroon, ulioiweka katika nafasi kwanza kwenye kundi I. Kwa jumla wana pointi 13 baada ya kucheza mechi sita.

Libya ilimaliza na pointi nne baada ya kuwasili mjini Yaounde na kuhitaji kushinda mechi hiyo ili kujipatia nafasi kwenye michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia.

Kwa sasa hivi Indomitable Lions wako kwenye mkondo mzuri kuelekea Brazil , lakini muhimu itakuwa kuwa waweze kushinda michuano hiyo ya kufuzu.

Washindi wengine walikuwa Algeria, Burkina Faso, Cape Verde, Egypt, Ethiopia, Ghana, Ivory Coast, Nigeria na Senegal.

Draw ya michuano ya kufuzu itafanyika mjini Cairo tarehe16 Septemba.