Kesi ya Mubarak kusikilizwa faraghani

Image caption Mfuasi wa Hosni Mubarak

Mahakama nchini Misri imeamuru vyombo vya habari kutohudhuria vikao vya kusikilizwa upya kwa kesi dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak.

Jaji Mahmoud el-Rachidi alisema kuwa vikao vitafanyika kati ya tarehe 19-21 Oktoba, na vitahusu maswala ya usalama wa kitaifa.

Bwana Mubarak, mwenye umri wa miaka 85,alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuhusika na mauaji ya waandamanaji wakati wa mapinduzi ya kiraia ya mwaka 2011.

Mawakili wa utetezi wanataka kulaumu vuguvugu la Muslim Brotherhood na vikosi vya usalama vya kimataifa kwa mauaji ya waandamanaji 850 kwenye vurugu hizo.

Mubarak alifungwa jela maisha Juni mwaka jana kwa kuhusika na mauaji hayo.

Lakini alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo na mahakama ikaamua kuzikiliza upya kesi hiyo.

Mubarak ameshtakiwa pamoja na wanawe wawili, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na maafisa sita wa usalama.

Hata hivyo vikao vyote vya kesi ya kwanza dhidi ya Mubarak vilifanyika faraghani. Lakini jaji Rachidi aliahidi kuwa wakati huu kesi hiyo itakapoanza upya itafanywa kwa uwazi mkubwa

Lakini aliamua Jumamosi kuwa waandishi wote wa habari watazuiwa kushuhudia kesi hiyo na pia wameharamishwa kuwanukuu mawakili.

Jaji alisema sababu kuu ya kesi kusikilizwa faraghani ni kutoa nafasi kwa mashahidi kutoa ushahidi wao .