Kanye West alimshambulia mpiga picha

Image caption Kanye West

Mwanamuziki wa kizazi kipya nchini Marekani Kanye West ameshtakiwa kwa kosa la jaribio la wizi baada ya kupigana na mpiga picha katika uwanja wa ndege mjini Los Angeles, Marekani.

Mpiga picha wa gazeti la udaku Daniel Ramos, alimshitaki West baada ya mwanamuziki huyo kumpiga usoni na kuitupa kamera yake chini.

Mawakili wa mwanamuziki huyo walisema kuwa alikuwa tu anajaribu kumzuia mpiga picha huyo kumpiga picha.

Ikiwa atapatikana na hatia huenda akafungwa jela miezi sita

Viongozi wa mashtaka walikataa kumshtaki West kwa makosa mabaya zaidi kuliko hilo kwa sababu mwathiriwa alipata majeraha madogo tu.

Tukio hilo lilitokea Julai tarehe 19 wakati waandishi wa magazeti ya udaku walikuwa wakimsubiri West kuwasili katika uwanja wa ndege.

Kanda ya video iliyonasa tukio hilo ilionyesha West akiwa ameghadhabishwa kwa sababu ya mpiga picha huyo kujaribu kumpiga picha.

Kisha baadaye aliripotiwa kumvamia bwana Ramos na kumpokonya kamera yake.

“Wakati Kanye aliponishambulia nilishtuka sana na nilipigwa na butwaa, Ramos aliwaambia waandishi wa habari.

"Nilimuuliza tu swali moja lakini nilishtuka sana aliponishambulia,’’ aliongeza kusema Ramos

Kanye atatakiwa kufika kwa mara nyingine mahakamani Oktoba 10