Rais Bashir aomba Viza kusafiri Marekani

Image caption Rais Omar el Bashir akiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum

Rais wa Sudan Omar al-Bashir, anayetakikana na mahakama ya ICC kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, ameomba hati ya usafiri kwenda nchini Marekani kwa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Mahakama ya kimataifa ICC, inamtaka Bashir kwa madai ya kuamuru mauaji ya halaiki na kuhusika na uhalifu wa kviita katika jimbo la Darfur.

Awali , vyombo vya habari vilisema kuwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Ali Karti ataongoza wajumbe wa nchi hiyo kuhudhuria mkutano huo mjini New York.

Mara ya mwisho kwa Bashir kuzuru Marekani ilikuwa mwaka 2006.

Kibali cha kukamatwa kwa Bashir kilitolewa Mei mwaka 2009 na Julai mwaka 2010. Mahakama ya ICC imemshitaki kwa makosa kumi ya uhalifu wa kivita , uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power, amethibitisha kuwa Marekani imepokea ombi la Viza kutoka kwa Rais Bashir.

Alitaja ombi hilo kama lisilofaa, la kuudhi na mzaha mkubwa kwa Marekani.

Msemamji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, alisema kuwa wanalaani juhudi za Bashir kutaka kusafiri kwenda Marekani.

"Kabla ya kuja katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, alisema Bi Harf kuwa , "Rais Bashir mwanzo anapaswa kujikabidhi kwa Mahakama ya kimataifa ya Hague kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu anayokabiliwa nayo.’’

Hata hivyo Bi Harf hakusema ikiwa Marekani itamnyima Viza Bashir.

Gazeti la Sudan la Tribune linasema kuwa Marekani huwa na mipango maalum ya kisheria kuwapa viza maafisa wanaotaka kuhudhuria shughuli za UN ,mjini New York.

Kinachoweza kufanyika ni kuwa Bashir anaweza kukamatwa ikiwa atadhubutu kuingia nchini Marekani akielekea UN. Licha ya hayo, mtu yeyote licha ya uraia wake hawezi kuzuiwa kuingia katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa

Mwezi jana Saudi Arabia ilikataa kuipa ruhusa ndege iliyokuwa imembeba Bashir kuruka katika anga yake wakati Bashir alipokuwa anasafiri kwenda nchini Iran