Marekani:Madai dhidi ya Syria yalikuwa sahihi

Image caption UN ilifanya utafiti wake kuthibitisha kuwa silaha za kemikali zilitumiwa Syria

Marekani , Uingereza na Ufaransa zinasema kuwa Ripoti ya Umoja wa Mataifa inayothibitisha kuwa silaha za kemikali zilitumiwa kuwauawa watu mjini Damscus imethibitisha msimamo wao kuwa Serikali ya Syria ndiyo yenye kulaumiwa kwa kutumia silaha hizo.

Mabalozi wa Marekani na Uingereza katika Umoja wa Mataifa walisema kuwa maelezo ya kina yalionyesha kuwa ni serikali pekee ambayo inaweza kulaumiwa kwa kutumia silaha hizo tarehe 21 mwezi Agosti.

Watu wengi waliuawa kwa kutumia silaha zenye sumu katika kitongoji kimoja mjini Damascus.

Urusi nayo imesema madai kwamba waasi walihusika hayawezi kupuuzwa.

Ripoti ilisema kemikali aina ya Sarin ilitumiwa kwenye roketi na kurushiwa watu wa kitongoji hicho. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon ametaja kitendo hicho kama cha unyama.

Sambulizi hilo liliifanya Marekani kutishia kuvamia Syria kijeshi ikiwa madai ya kutumia silaha hizo yatathibitishwa.