Jeshi la Nigeria lawaua wapiganaji 150

Image caption Wanajeshi 9 wangali hawajulikani waliko baada ya makabiliano makali kuzuka kati ya wapiganaji na wanajeshi hao mjini Borno

Jeshi la Nigeria, linasema kuwa limewaua wapiganaji 150 wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram wakati wa msako dhidi yao wiki jana.

Makabiliano yalitokea wakati jeshi lilipokuwa linafanya msako dhidi ya wapiganaji hao katika jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Katika taarifa yake, jeshi lilisema kuwa takriban wanajeshi 16, walifariki wakati walipofanya shambulizi la kwanza dhidi ya kambi ya wanajeshi hao ambako walipata silaha nzito

Wanajeshi wengine wa serikali wanasemekana kutojulikana waliko. Aidha jeshi lilisema pia liliweza kumuua kamanda wa wapiganaji hao Abba Goroma.

Mwandishi wa BBC nchini Nigeria anasema kuwa, jeshi kwa kawaida huongeza chumvi idadi ya wapiganaji waliouawa kwa lengo la kuonyesha kuwa wanajeshi waliouawa kwenye mapigano walikuwa wachache.

Boko Haram ilianza harakati zake mwaka 2009 katika jimbo la Borno ambalo hadi sasa liko chini ya sheria ya hali ya hatari.