Tetemeko la ardhi lawaua 270 Pakistan

Image caption Zaidi ya watu 300 wamejeruhiwa

Tetemeko kubwa la ardhi limewauwa watu 270 katika mkoa wa Kusini Magharibi wa Balochistan nchini Pakistan.

Tetemeko hilo la kipimo cha 7.7-lilipiga Jumaanne alasiri . Nyumba nyingi zilibomolewa na watu wengi walipaswa kulala nje.

Baada ya tetemeko hilo ,kisiwa kidogo kiliibuka nje ya mwambao karibu na bandari ya Gwadar.

Watu walikusanyika ufukweni kushuhudia kisiwa hicho kipya ambacho kinakadiriwa kua na urefu wa mita 200 na upana wa mita 100 na kiinuka mita 20 kutoka upeo wa bahari .

Balochistan ndio mkoa mkubwa wa Pakistan lakini ukiwa na watu wakaazi wachache kupita yote

Eneo hilo hukumbwa na mitetemeko ya mara kwa mara na mnamo mwezi wa Aprili watu 35 waliuwawa katika tetemeko ambalo kitovu chake kilikua Kusini Mashariki mwa Iran mnamo mwezi wa April.

Vibanda vya udongo

Tetemeko hilo lilikua la nguvu hata watu wa miji iliyo mbali ya Karachi, Hyderabad, na mji mkuu wa India, Delhi walihisi mtikisiko wake.

Vijiji vizima inaarifiwa vilifyekwa katika wilaya ya wakaazi masikini ya Awaran

Msemaji wa serikali ya Balochistan, Jan Buledi, amesema waliopatwa na maafa zaidi ni katika mji wa Awaran na vijiji vinavyouzingira na ameonya idadi ya vifo huenda ikaongezeka. Takriban watu 340 wamejeruhiwa.

Msemaji huyo amesema kuna ukosefu mkubwa wa huduma za matibabu na hospitali hazina nafasi za kutosha kuwatibu majeruhi .

Alisema helikopta zinawasafirisha majeruhi mahututi hadi mjini Karachi na wengine wanahudumiwa katika wilaya jirani.

Jeshi la Pakistan lilikua miongoni mwa makundi ya kwanza kutoa msaada kwa kua tayari limekua huko miaka kadhaa sasa kwa sababu ya uasi wa watu wanaotaka kujitenga kwa mkoa huo wa Balochistan.

Jeshi limesema limetuma zaidi ya wanajeshi 200 , wana matibabu na mahema kutoka mji mkuu wa mkoa huo Quetta, lakini shughuli za uokozi zinatatizwa kwa hali ya milima ya eneo hilo.