Maandamano Sudan kupinga kuondolewa ruzuku

Image caption Waandamanaji wanapinga hatua ya serikali kuondoa ruzuku ya mafuta

Polisi nchini Sudan wamewatifulia gesi ya kutoa machozi waandamanaji katika Mji Mkuu Khartoum, huku wengi wakiendelea kukasirishwa na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.

Walioshuhudia maandamano hayo walisema kuwa waandamanaji waliteketeza jengo moja la Chuo Kikuu na vituo kadhaa vya petroli. Pia waliziba njia kuu ya kuelekea uwanja wa ndege.

Watu wawili wameuawa tangu maandamano hayo kuanza Jumatatu wakati Serikali ilipotangaza kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.

Hatua hiyo imefikiwa katika juhudi za serikali kuongeza mapato ya Serikali.

Hata hivyo waandishi wa habari hapo mjini wanasema kuwa hatua hiyo imewaathiri zaidi watu wa mapato ya chini na kuzusha Serikali kuchukiwa na raia wa kawaida.

Duru zinasema kuwa watu watatu wamefariki kutokana na ghasia hizo. Waziri wa elimu naye amesema kuwa shule ziliko katika mji mkuu zitasalia kufungwa hadi Septemba tarehe 30.

Kwa mujibu wa shirika la AFP, watumijai wa mtandao wa internet wanasema kuwa huduma zimekatizwa ingawa haijulikani ikiwa ni hatua ya serikali kudhibiti mawasiliano au ilitokana na hitilafu za kimitambo.

Serikali ilitangaza Jumatatu hatua zaidi za kupandisha bei ya mafuta baada ya kusitisha ruzuku kwa muda katika juhudi za kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini humo.

Mnamo siku ya Jumanne waandamanaji waliteketeza ofisi za chama tawala,mjini Omdurman.