ICC kuamua rufaa ya Taylor leo

Image caption Charles Taylor akiwa mahakamani ICC

Mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa The Hague, inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu rufaa aliyokata rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor.

Mnamo mwezi Mei, mahakama hiyo ilimuhukumu Talor miaka hamsini gerezani kwa kusaidia haratakati za waasi katika nch jirani ya Sierra Leone wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1991 na 2002.

Taylor alikuwa rais wa kwanza wa zamani kuhukumiwa na mahakama ya kimataifa ya ICC kwa uhalifu wa kivita tangu vita vya pili vya dunia.

Mawakili wake wanataka aachiliwe wakiteta kuwa kulikuwepo makosa ya kisheria na ukweli wakati wa kesi yake.

Hata hivyo, upande wa mashtaka unasema kuwa unataka kuongeza hukumu yake hadi miaka 80.

Mwandishi wa BBC mjini The Hague anasema kuwa uamuzi wa mahakama utatizamwa kwa karibu kwa sababu watu walisifu sana hukumu aliyopewa Taylor wakisema kumbe hata watu walio katika nyadhifa za juu wanaweza kukabiliwa na sharia.

Charles Taylor,mwenye umri wa miaka 65, alipatikana na hatia kwa kusaidia waasi wa Sierra Leone kufanya ugaidi, ubakaji , mauaji na kutumia watoto kama wanajeshi.

Pia alipatikana na hatia ya kupanga badhi ya mashambulizi ya waasi katika nchi jirani ya Sierra Leone wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Alikamatwa mwaka 2006 lakini alisisitiza kuwa hakuwa na hatia wakati wa kesi hiyo.

Ikiwa mawakili wa Taylor watashindwa katika rufaa yao , atatumikia kifungo chake katika nchi ya kigeni. Uingereza imeitikia kumkubali Taylor kutumikia kifungo chake nchini humo.

Nchi zingine ambako Taylor anaweza kutumikia kifungo chake ni Sweden au Rwanda.