Kenya iko vitani na al-Shabaab

Wakenya wakiomboleza kwa kuwasha mishumaa nje ya Westgate

Serikali ya Kenya imesema nchi iko katika vita na wapiganaji wa Somalia, al Shabaab.

Imekanusha kuwa vitisho vya mashambulio vinavotolewa na kundi hilo vilipuuzwa.

Inajulikana kuwa watu 67 walikufa katika shambulio la Westgate, liloendelea kwa siku nne.

Jumamosi usiku wafiwa na marafiki walioonesha majonzi waliwasha mishumaa nje ya Westgate kuwakumbuka waliokufa.

Magazeti ya Kenya yameandika ilani inayodaiwa kutolewa na idara ya usalama mwaka mmoja uliopita kuhusu watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa al-Shabaab mjini Nairobi ambao wakipanga mashambulio ya kujitolea mhanga, piya katika jengo la maduka la Westgate.

Magazeti ya Kenya yameuliza iwapo wakuu walishindwa kuchukua hatua baada ya onyo hilo na mengine yaliyofuata; pamoja na onyo moja kwamba kutafanywa mashambulio sambamba mijini Nairobi na Mombasa baina ya tarehe 13 hadi 20 Septemba.

Kamati ya bunge itayokutana Jumatatu imeonesha inataka kutazama swala hilo la ilani hizo zilizotolewa.

Afisa mmoja mwandamizi wa wizara ya mambo ya ndani alisema serikali inapata taarifa kama hizo kila siku.

Hatua zimechukuliwa kuepusha mashambulio mengi.

Alisema Kenya iko vitani, na kila siku kijana wa Kenya anashawishiwa na al-Shabaab kuuwa Wakenya.