Kenya - Bila usalama Somalia, hatutoki !

Image caption Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta atoa Onyo kali kwa magaidi

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa majeshi ya Kenya yataendelea kukaa Somalia hadi usalama utakapoimarishwa katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya miaka mingi.

Rais Kenyatta amesema kuwa nchi yake haitashurutishwa na magaidi walioteka jengo la maduka la Westgate kwa siku 4.

Rais Kenyatta alihutubia umati uliokusanyika kwa maombi ya pamoja ya dini mbali mbali, kwa ajili ya watu 67 waliouawa katika shambulio la Westgate.

Shambulio hilo ndio baya zaidi kuwahi kutokea nchini Kneya tangu majeshi yake yaingie nchini Somalia mwaka wa 2011.

''Hawa wauaji waliokuja kutenda ukatili wao ulio na woga hapa nchini kwetu, walikuwa wanadai kuwa wanafanya hivyo kwasababu majeshi ya Kenya yapo nchini Somalia. Nataka niwaeleze bayana kuwa, majeshi yetu yatakaa huko hadi kuwepo amani katika nchi hiyo.''

Mmoja wa makasisi walioongoza maombi hayo, alisema,'' Baba tunakuomba utawale nchi hii. Na uwaoneshe maadui wote wa taifa hili kuwa wewe unaipenda nchi hii na jina lako litatukuzwa.''

Wapiganaji hao wa Al Shabaab wamesema kuwa walifanya shambulio hilo kulipiza kisasi kwa namna majeshi ya Kenya yaliingia na kuwapiga nchini Simalia.

Rais Kenyatta pia ametangaza kuwa serikali itaunda tume maalum kuchunguza upungufu mkubwa uliojitokeza kwa vyombo vya usalama kufuatia shambulio la Westgate.

''Tutaunda pia tume maalum kuangalia ni wapi tulikosea, ili tujirekebishe kuendelea mbele. Tuone ni wapi kumetokea upungufu na ni vipi tutarekebisha.''

Ushirikiano

Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria maombi hayo. Bwana Odinga ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuisaidia Kenya kukabili ugaidi.

Aliongeza kuwa ni makosa kwa mataifa ya magharibi kutoa tahadhari kwa raia wao kutotembelea Kenya huku kwa upande mwingine zikishinikiza Kenya kufayia mabadiliko idara zake za usalama.

Bwana Odinga amesisitiza kuchukuliwa hatua za kuimarisha usalama nchini Kenya.

''Shambulio hili ni ishara kuwa tunaingia katika makabiliano makali zaidi. Ni lazima tubadilishe mbinu zetu za kukusanya intelijensia na uharaka wa kuchukua hatua. Ni lazima pia tuweke adhabu kali kwa maafisa wanaolinda mipaka yetu ambao wanakubali mlungula na kuruhusu maadui kuingia nchini na kutuumiza.''

Mwandishi wa BBC anasema kuwa wakenya walivyojitokeza kwa wingi, walitaka kuonesha ishara ya utangamano wa dini mbali mbali licha ya tofauti za imani.

Wiki moja baada ya shambulio la Westgate kumalizika, watu 39 wameripotiwa kutoweka.