ICC yamsaka mshirika wa Gbagbo

Image caption Bwana Ble anashukiwa kufanya mauaji, ubakaji, mateso na vitendo vingine vya kinyama

Mahakama ya kimataifa ya ICC, imetangaza rasmi kutoka kibali cha kumkamata aliyekuwa waziri wa Ivory Coast,Charles Ble Goude kwa madai ya uhalifu wa kivita.

Anatakikana na mahakama hiyo kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi ambazo zilizuka kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata mwaka 2010 nchini Ivory Coast.

Takriban watu 3,000 waliuawa katika ghasia hizo ambapo aliyekuwa rais Laurent Gbagbo alikuwa amekataa kuondoka mamlakani baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu.

Bwana Ble Goude amekanusha madai ya kuongoza makundi ya vijana waliokuwa wanamuunga mkono Gbagbo kufanya mashambulizi mabaya dhidi ya wenzao.

Kibali hicho cha kumkamata , kilitangazwa mara ya kwanza Disemba mwaka 2011 lakini sasa ndio kimetangazwa rasmi hadharani na kinamtaja bwana Ble Goude kama mshirika wa karibu sana wa Gbagbo.

Mahakama ya ICC imesema kuwa Ble mwenye umri wa miaka 40 ambaye kwa sasa anazuiliwa Ivory Coast, anashukiwa kwa kufanya mauaji, ubakaji, mateso na vitendo vingine vya kinyama kati ya Disemba mwaka 2010 na Aprili mwaka 2011.