Miradi ya EU nchini DRC yakosolewa

Image caption Wanawake wakipokea mafunzo kuhusu afya ya watoto

Miradi mingi inayofadhiliwa na muungano wa Ulaya kwa madhumuni ya kuimarisha demokrasia na uongozi bora katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imekosa kufaulu.

Hii ni kwa mujibu wa wakaguzi wa hesabu kutoka Muungano huo.

Mahakama ya wakaguzi wa hesabu wa Ulaya wanasema kuwa Muungano wa Ulaya unahitaji kuboresha ambavyo miradi inaendeshwa ili iwe na faida, katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ukaguzi wao ulichunguza matumizi ya pesa katika miradi iliyofanywa kati ya mwaka 2003-2011, wakati ambapo EU ilitoa msaada wa dola bilioni 2.6 kwa DRC.

Taifa hilo lenye utajiri wa madini linakumbwa na umaskini, ufisadi na mizozo chungu nzima.

Majeshi ya Congo kwa ushirikiano na yale ya UN, yanapambana dhidi ya waasi wa M23 karibu na mji wa Mashariki wa Goma.

Kwa miaka mingi, maafisa wa utawala katika mji mkuu Kinshasa, wamekuwa na wakati mgumu kukabiliana na uasi na kuiunganisha nchi.

Lakini katika jibu lake kwa wakaguzi hao, Kamishna mkuu wa ustawi amesema kuwa ni mapema sana kutoa hukumu dhidi ya miradi ambayo bado hata haijakamilika.

Alidokeza kuwa hatua zimepigwa katika kufanyia mageuzi idara ya polisi na tume ya uchaguzi lakini kazi ya ziada bado inahitajika.

Wakaguzi hao wanasema kuwa chini ya nusu ya miradi iliyokaguliwa imeweza kutimiza malengo yao au inatarajiwa kufanya hivyo.

Walikosoa muundo wa miradi ya Muungano wa Ulaya inayolenga kuimarisha uongozi bora nchini DRC wakisema kuwa mahitaji ya raia hayajafanyiwa uchunguzi ipasavyo.

Pia wameutaka muungano huo kuhakikisha kuwa miradi hiyo inachunguzwa kwa karibu sana kuhakikisha kuwa pesa hazikufujwa.