Magaidi Kenya huenda hawakuwa wa kigeni

Image caption Ghorofa tatu za jengo la Westgate ziliporomoka

Maafisa wa ujasusi nchini Kenya wanaochunguza shambulizi la kigaidi lililotokea mwezi jana katika jengo la Westgate, wanasema dalili zinaonyesha kuwa huenda waliofanya mashambulizi hayo ni wanachama wa mtandao wa kigaidi nchini Kenya

Mwandishi wa BBC anasema kuwa madai ya awali kuwa magaidi hao walitoka nje ya Kenya yanaonekana kutokuwa na msingi.

Duru za kiusalama pia zimeambia BBC kuwa wanajeshi walipoingia katika jengo la Westgate walifyatua risasi kiholela na kwa muda mrefu na kuhatarisha maisha ya raia na polisi waliokuwa ndani ya jengo hilo.

Pia kuna ripoti za wanajeshi kupora maduka yaliyokuwa ndani ya jengo hilo. Watu 67 waliuawa na wengine zaidi ya miamoja sabini kujeruhiwa. Hadi sasa watu 39 hawajulikani waliko.

Kundi la kigaidi la Al-Shabab limekiri kutekeleza mashambulizi hayo.

Madai ya awali ya maafisa wa ujasusi kuwa wanamgambo wenye uraia wa uingereza walikuwa miongoni mwa wavamizi hayajapatikana kuwa na msingi.

Kuna ushahidi kuwa wanamgambo wa kisomali wa Al Shabab wamevuka mipaka na kuingia nchini humo kwa shughuli ya kuwasajili wapiganaji vijana kwa lengo la kuwapa mafunzo ya kigaidi.