Ungereza na Uturuki hazikuvamia Barawe

Wapiganaji wa al-Shabaab nchini Somalia

Wanachama wa kundi la al-Shabaab nchini Somalia wanasema kuwa mji wao kusini mwa Somalia umeshambuliwa na wanajeshi wa mataifa ya Magharibi.

Wapiganaji hao wanasema wanajeshi wa kigeni waliuvamia mji wa Barawe usiku wa manane.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema mpiganaji mmoja aliuwawa na risasi nyingi zilifyatuliwa.

Baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa helikopta ilitumiwa kwenye shambulio hilo.

Wengine wanaeleza kuwa wanajeshi waliingia usiku wakitokea pwani.

Al Shabab ilisema shambulio hilo halikufanikiwa ingawa inakiri mpiganaji wao mmoja aliuwawa.

Kundi hilo linadai kuwa wanajeshi maalumu wa Uingereza na Uturuki ndio waliofanya shambulio lakini hayo yamekanushwa na Uingereza na Uturuki.

Kundi la al Shabaab limesema kuwa lilifanya shambulio la mwezi uliopita mjini Nairobi dhidi ya jumba la maduka ambalo kwa sehemu linamilikiwa na Muisraili.

Miaka mine iliyopita jeshi la wanamaji wa Marekani liliuvamia mji wa Barawe kumuuwa mtu aliyeshukiwa kuwa mfuasi wa al-Qaeda.