Maiti zaidi zapatikana Lampedusa

Kazi za uokozi zaanza tena Lampedusa

Wakuu wa Utaliana katika kisiwa cha Lampedusa wanasema wameopoa miili zaidi kutoka meli iliyozama Alkhamisi.

Inakisiwa wakimbizi kutoka Afrika zaidi ya 300 walikufa katika ajali hiyo.

Miili 10 iliopolewa katika mbizi ya kwanza hii leo lakini kwa vile meli iko chini ya kina kirefu cha maji, wazamia mbizi wanaweza kubaki majini kwa dakika tu kabla ya kuja juu kupumua.

Afisa aliyehusika piya katika kazi za uokozi - Mauro Casinghini - alisema ana hakika miili iliyobaki itapatikana:

"Sifikiri ni tatizo kubwa kuipata miili.

Miili imenasa ndani ya boti kwa hivo pengine katika shughuli hizi tutaweza kuipata miili yote iliyonasa humo.

Hatujui itakuwa katika hali gani lakini uzoefu umetufunza kwamba miili, au mabaki ya miili, itapatikana."

Na waziri wa mshikamano wa Utaliana, Cecile Kyenge, aliliambia gazeti moja la Utaliana kwamba nchi lazima itafute makaazi zaidi ya wakimbizi kumudu wimbi la wakimbizi kutoka maeneo ya vita ya Afrika na Mashariki ya Kati.