Waziri mkuu wa Libya Zaidan aachiliwa

Image caption Zeidan alitoa wito kwa Marekani kusaidia Libya kupambana na wapiganaji wa kiisilamu

Waziri mkuu wa Libya Ali Zeidan aliyeripotiwa kutekwa nyara na waliokuwa waasi katika jiji kuu la Libya Tripoli mapema hivi leo ameachiliwa.

Maafisa wamenukuliwa wakisema kuwa hakuumizwa.

Tukio hilo limeshutumiwa na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague.

Ali Zeidan alitekwa nyara na kundi la waasi waliokuwa na uhusiano na serikali kwa jina Revolutionaries Operations Room.

Walisema walimteka nyara kwa maagizo ya mwendesha mkuu wa mashitaka ingawa wizara ya sheria imekanusha madai hayo.

Kundi hilo lilikuwa miongoni mwa makundi ya wapiganaji walioghadhabishwa na hatua ya makomando wa Marekani kumkamata Anas Al-Liby mshukiwa wa kundi la kigaidi la al-Qaeda .

Wengi walitaja hatua ya Marekani kama ya kuingilia uhuru wa taifa hilo na hata kutaka maelezo kutoka kwa balozi wa Marekani nchini humo.

Image caption Picha ya Zeidan akitekwa nyara mjini Tripoli

Mwandishi wa BBC mjini humo anasema Zeidan alitekwa nyara akiwa ndani ya hoteli ya kifahari anamoishi.

Serikali imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kali baada ya makomando wa Marekani kumkamata mmoja wa viongozi wa al-Qaeda Anas al-Liby nchini Libya.

Bwana Liby alikamatwa Jumamosi mjini Tripoli kwa madai ya kuhusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 2008.

Mnamo siku ya Jumatatu Libya ilimhoji balozi wa Marekani kuhusu kukamatwa Al Liby.

Kwa upande wake Zeidan alitoa wito kwa Marekani na nchi za Magharibi kuisaidia serikali ya Libya kukomesha vitendo vya wapiganaji wenye itikadi kali nchini humo.

Kwenye mahojiano na BBC, alisema kuwa Libya inatumiwa kama kambi ya kuweka silaha.

Waziri mkuu aliambia BBC kuwa nchi yake inatumia kama kivukio cha kusafirishia silaha kwenda katika maeneo mengine ya kanda hiyo.