Taliban tayari kwa mazungumzo Pakistan

Image caption Taliban wako tayari kwa mazungumzo ila wataendelea kushambulia maslahi ya Marekani

Kiongozi wa Taliban nchini Pakistan Hakimullah Mehsud ameambia BBC kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na serikali ingawa amesisitiza kuwa bado serikali haijamshauri.

Katika mahojiano ya kipekee, alikanusha kufanya mashambulizi ya hivi karibuni katika maeneo ya umma na kusema kuwa ataendelea kushambulia mashlahi ya Marekani na washirika wake. Kiongozi huyo huongoza makundi zaidi ya 30 ya Taleban katika maeneo wanakoendeshea harakati zao.

Baada ya kuchaguliwa mnamo mwezi Mei, Waziri mkuu, Nawaz Sharif alitangaza kuwa atafanya mazungumzo na Taliban bila vikwazo.

Kundi hilo limewaua maelfu ya watu katika vita vyake dhidi ya serikali ya Pakistan katika miaka ya hivi karibuni.

Wanadhibiti maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, na wamelaumiwa kwa mashambulizi ya kujitoa mhanga.

Wakati baadhi ya wapiganaji wa Taliban wanashuku kuwa mazungumo hayo ni njama ya kuwakamata, wengi wana matumaini kutokana na ombi la mara kwa mara la serikali, kufanya mazungumzo.

Wiki jana baraza kuu laTaliban lilituma ujumbe kwa mirengo yote ya Taliban kupata maoni yao kuhusu jambo hilo lakini bado wanasubiri majibu.

Mwandishi wa BBC Ahmed Wali Mujeeb alimuhoji Hakimullah Mehsud katika eneo la siri mwezi huu nchini Pakistan.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa mazungumzo ya amani na serikali, Mehsud alisema kuwa wanaamini inaweza kufanyika ila serikali bado haijawashauri. Alisema serikali inahitaji kuketi nao kisha watoe masharti yao ya kusitisha vita na kuwa hayuko tayari kwa mazungumzo hayo kufanyika kupitia kwa vyombo vya habari.