AU yalaani ICC kwa uonevu Afrika

Image caption AU inajadili swala hili baada ya ICC kupuuza ombi la kutaka kuhamisha kesi za Kenyatta na Ruto

Mawaziri wa mambo ya nje Afrika wanakutana mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili uhusiano wa bara la Afrika na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia Tedros Adhanom Ghebreyesus ameilaani mahakama ya ICC kwa kusema ina mapendeleo sana na hicho sio kitu kinachokubalika na kuwa ina uonevu kwa nchi za Afrika.

Waziri huyo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao maalum cha AU kuhusu mahakama ya ICC.

Kikao hicho kinafuatia ombi la serikali ya kenya.

Umoja wa Afrika unaishtumu mahakama ya ICC kwa kuwalenga viongozi wa bara hilo huku ikipuuzilia mbali uhalifu mwengine dhidi ya binadamu unaotekelezwa katika maeneo mengine ulimwenguni.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho waziri wa maswala ya kigeni kutoka Ethiopia Tedros Adhanom ameishtumu mahakama hiyo kwa kukataa kuheshimu uwezo wa marais wa bara Afrika na kukitaka kikao hicho kushutumu mahakama hiyo.

Aidha amekitaka kikao hicho kuwasilisha ombi la kuahirisha kesi zinazowakabili Rais wa kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake Wiliam Ruto kusikizwa katika mahakama hiyo.

Mkutano huu maalum umeitishwa baada ya ICC kukataa ombi la wanachama 34 wa Muungano wa Afrika kurejesha kesi za Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto nyumbani.

Miongoni mwa yatakayozungumziwa ni hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo.

Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana kati ya ICC na AU, viongozi wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya AU katika kile kinachosemekana ni kutafakari upya uhusiano wa bara hilo na mahakama ya ICC.

Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya ICC imekosa kushughulikia ombi lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za Kenya. AU inasema kuwa ICC ina njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa kiafrika.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu katika mahakama hiyo.

Kesi yao inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1100 waliuawa.

Hata hivyo viongozi hao wamekanusha madai hayo.

Bunge la Kenya ambalo lina idadi kubwa ya wabunge wa mrengo wa Jubilee unaotawala nchi, tayari lieanzisha hoja ya kuondoa Kenya kutoka katika mahakama ya ICC.

Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza nchi za Afrika kujadili hoja ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na majirani zake kama Uganda na Rwanda.

Naibu mwenyekiti wa AU Erastus Mwencha, ameambia BBC kuwa swala hilo sasa ni zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.

Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa huenda AU isikubali kwa ujumla kujiondoa ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na Botswana tayari zimepinga hatua ya kujiondoa ICC.