ICC: Kesi ya Senussi ifanyike Libya

Image caption Senussi alikuwa mshirika wa karibu sana wa Gadaffi

Mahakama ya kimataifa ya jinai, ICC, imeamua kuwa aliyekuwa mkuu wa ujasusi wakati wa utawala wa marehemu Muamar Gadaffi, Abdullah al-Senussi, afunguliwe mashtaka nchini Libya.

Uamuzi huu una maana kuwa ICC haitaendelea kumtaka tena Bwana Senussi kwenda Hague kwa kesi dhidi yake.

Senussi aliyekuwa mkuu wa ujasusi alitakikana na mahakama ya ICC kwa uhalifu dhidi ya binadamu , makosa aliyoyafanywa wakati wa mapinduzi ya kiraia dhidi ya Gaddafi.

Bwana Senussi alikabidhiwa na Mauritania kwa Libya baada ya kukamatwa nchini humo mwaka jana.

Mahakama ya ICC kawaida haiendeshi kesi dhidi ya mshukiwa ikiwa kuna dalili kwamba watatendewa haki nchini mwao.

Aidha katika taarifa yake mahakama hiyo imesema kuwa uamuzi huo hauna uhusiano wowote na kesi dhidi ya mwanawe marehemu Gaddafi,Saif al-Islam Gaddafi anayetakikana na mahakama hiyo.

Islam pia alishtakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita na alishitakiwa pamoja na watu wengine 36.

Saif Gaddafi anazuiliwa na kundi la wapiganaji wa kiisilamu mjini Zintan. Mwezi jana wapiganaji hao, walikataa kumkabidhi Seif kwa serikali kuweka kufikishwa mahakamani pamoja na Senussi .