Viongozi madarakani wasifikishwe ICC

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nee wa Ethiopia, Tedros Adhanon Ghebreyesus,  katika mkutano wa AU

Viongozi wa Afrika wanakutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo swala kubwa ni uhusiano wa Umoja wa Afrika na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, alisema siyo kusudi la mkutano huo kuipiga vita ICC, lakini ni wito kwa mahakama hayo kuzingatia wasiwasi wa Afrika kwa makini.

Alisema kesi za ICC dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Omar al-Bashir wa Sudan ambao wanakabili mashtaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu, zinaweza kuzuwia juhudi za kuleta amani na mapatano katika nchi zao.

Mkutano unatarajiwa kuuomba Umoja wa Mataifa kusimamisha kwa muda kesi za ICC dhidi ya viongozi wa Afrika walioko madarakani.

Lakini inaonesha viongozi katika mkutano wamelitupilia mbali pendekezo kwamba Afrika ijitoe kabisa wenye ICC.

Viongozi maarufu wa Afrika - kama katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kutoka Ghana - wameshikilia kuwa Afrika yenyewe siyo inayofikishwa mahakamani ICC, bali kesi ni dhidi ya tabia ya wanasiasa kufanya watakalo.