Pwani za Ulaya ni makaburi

Mashua ya Malta ikiokoa wakimbizi nje ya Lampedusa

Waziri Mkuu wa Malta, Joseph Muscat, amesema pwani za Ulaya zilioko karibu na Afrika zimegeuka viunga vya makaburi, baada ya mashua nyengine iliyojaa wakimbizi kuzama.

Katika tukio la karibuni watu kama 50 wamezama kusini ya kisiwa cha Lampedusa, Utaliana.

Walinzi wa pwani wa Malta na Utaliana waliwaokoa watu 200, wakifanya kazi hiyo usiku kucha.

Waziri Mkuu wa Utaliana, Enrico Letta, amesema ajali hiyo ni thibitisho jengine kubwa kuhusu hali ya dharura ilioko Mediterranean.

Juma lilopita wakimbizi zaidi ya 330 walikufa baada ya mashua yao kuzama karibu na Lampedusa.