Upinzani wa Syria hautaki kuzungumza

George Sabra

Kiongozi wa kundi kubwa katika ushirikiano wa upinzani nchini Syria amesema ana hakika hatohudhuria mazungumzo ya amani ambayo Marekani, Urusi na Umoja wa Mataifa zinataraji kufanya kati ya mwezi Novemba.

George Sabra, kiongozi wa kundi la Syrian National Council, SNC, ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba kundi lake litatoka katika ushirikiano wa upinzani iwapo ushirikiano utaamua kuhudhuria.

Kundi la SNC awali lilikuwa ndilo kundi kubwa kabisa la upinzani.

Mwaka jana lilijiunga na makundi mengine na kuwa ushirikiano; lakini bado ni kubwa kabisa katika upinzani.

Sasa kiongozi wake, George Sabra, amesema SNC imeamua kabisa kwamba haitoshiriki kwenye mazungumzo yaliyopendekezwa ikiwa Bashar al-Assad bado yuko madarakani.

Matamshi yake hayo yamekuja wakati Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, John Kerry, anajitayarisha kukutana na mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa na Jumuia ya Nchi za Kiarabu,

Lakhdar Brahimi, mjini London Jumatatu.

Umoja wa Mataifa, Urusi na Marekani, wote wanataraji kuandaa mazungumzo ya Geneva yaliyopangwa kufanywa kati ya Novemba.

Huku nyuma serikali ya Syria, ambayo inaungwa mkono na Urusi, imesema iko tayari kwenda Geneva.

Tamko la George Sabra linaonesha kazi kubwa inayokabili Marekani ikijaribu kupata ujumbe wa kuaminika wa upinzani kushiriki kwenye mazungumzo.