109 wafariki tamashani India

Image caption Baadhi ya jamaa za wale waliofariki kutokana na mkanyagano wa watu India

Idadi ya watu waliofariki katika msongamano wa watu wakati wa tamasha la kihindi, katika mji wa Madhya Pradesh, imepanda na kufika watu 109.

Maafisa wenyeji wanasema kuwa watu wengi walifariki baada ya kutokea mkanyagano karibu na hekalu la Ratangarh viungani mwa mji wa Datia. Wengine walifariki waliporuka kutoka katika daraja hiyo.

Wakati huo huo, miili ya watu hao imechomwa usiku kucha kama ilivyo desturi ya wahindi kwani kwa kawaida hawaziki mtu bali wanachoma mwili wake.

Maelfu ya watu walikusanyika kwa tamasha hilo la Navrata lililodumu siku tisa.

Aidha maafisa walisema kuwa mkanyagano huo ulisababishwa na tetesi kuwa daraja hiyo ilikuwa karibu kuanguka kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwepo.

"taarifa tulizonazo zinasema kuwa watu 109 wamethibitishwa kufariki na 133 kujeruhiwa,'' shirika la habari la AFP lilimnukuu Anand Mishra, afisaa mmoja wa polisi akisema siku ya Jumatatu.

"tulipata baadhi ya miili kutoka kwenye mto na kutoka sehemu walizokuwa wamekanyagiwa hadi kufa,'' alisema bwana Mishra .

Ajali hii ilitokea siku ya Jumapili na wengi wa waathiriwa walikuwa wanawake na watoto.

Daraja hiyo ina urefu wa mita 500 na ilikuwa imejengwa upya baada ya kutokea msongamano mwingine wa watu mwaka 2007.

Kwa sasa jambo muhimu limekuwa kuwapa mahitaji muhimu wale waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo.

Tamasha za kihindi nchini India zinasifika sana kwa misongamano na hata watu kufariki.

Mwaka jana pekee mamia pia walifariki katika ajali tatu sawa na hii.

Mnamo mwaka 2011 zaidi ya watu 100 walifariki katika tamasha lengine katika jimbo la Kerala.