Mazungumzo yaanza kuhusu nuklia ya Iran

Image caption Wajumbe wa mazungumzo ya mpango wa nuklia wa Iran

Mataifa makubwa duniani yameanza mazungumzo yao ya kwanza na Iran kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo tangu Bwana Hassan Rouhani kuwa Rais wa Iran mwezi Agosti mwaka huu.

Akionekana kuwa kiongozi mwenye msimamo wa kadiri, Bwana Rouhani amesema anataka makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yawe yamekamilika katika kipindi cha miezi sita,ambayo yanazishirikisha Marekani, Urusi, Uchina, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.

Hakuna kinachotarajiwa kufikiwa katika siku mbili za mazungumzo hayo yanayofanyika mjini, Geneva, Uswisi, lakini waziri wa mambo ya nje wa Iran anasema ana matumaini kwamba mwelekeo wa mazungumzo hayo utaafikiwa.

Mataifa ya magharibi yaliishuku Iran kuwa ilikuwa inatafuta uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia kupitia mpango wake huo.

Iran imekuwa ikikanusha tuhuma hizo na kusema kwamba, mpango wake wa nyuklia ni kwa matumizi salama.

Mazungumzo haya rasmi ni ya kwanza kufanyika tangu Rais Hassan Rouhani aingie madarakani miezi miwili iliyopita na kuonyesha matumaini ya kupatikana kwa suluhisho la mgogoro huu wa muda mrefu. Iran imeahidi pendekezo jipya kuhusu mpango wake wa nyuklia utaziwezesha pande zote kufikia muafaka.

Hata hivyo Israel imeyataka mataifa ya magharibi kutolegeza vikwazo vyao dhidi ya Iran hadi hapo itakapothibitisha kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi salama