Mamia wafariki wakiwa wamezuiliwa Nigeria

Image caption Jeshi la Nigeria limekuwa likipambana dhidi ya Boko Haram

Mamia ya watu wamefariki katika vituo vya kuwazuilia washukiwa wa uhalifu Kaskazini Mashariki mwa Nigeria huku jeshi likijaribu kupambana vikali na kundi la wapiganaji wa kiisilamu Boko Haram katika eneo hilo.

Shirika la kimataifa la Amnesty International linasema kuwa vifo vya baadhi ya vimetokana na msongamano kwenye magereza na wengine kutokana na kukosa chakula na mauaji ya kiholela.

Shirika hilo linaitisha uchunguzi wa haraka kuhusiana na vifo hivyo.

Serikali, hata hivyo haijatoa kauli rasmi kuhusu ripoti ya Amnesty.

Lakini jeshi la Nigeria limekanusha madai hayo na mengine ya awali kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu.

Afisaa mmoja mkuu wa jeshi aliambia Amnesty kuwa takriban watu 950 walifariki kwenye operesheni ya kijeshi, mapema mwaka huu.

Wengi walisemekana kuwa uhusiano na kundi la Boko Haram.

Boko Haram inapigana dhidi ya serikali ya Nigeria ikitaka kubuni utawala wa kiisilamu na imefanya mashambulizi kadhaa katika shule za umma.

Takriban wanafunzi 50 waliuawa mapema mwezi huu wakiwa kwenye mabweni yao katika shambulizi ambalo kundi hilo lililaumiwa kutekeleza.

Hali ya hatari ilitangazwa katika majimbo matatu ya Kaskazini mwezi Mei , ikiwemo Yobe, Borno na Adamawa kama hatua ya kuzuia mashambulizi yanayofanywa na Boko Haharam.