Taylor apelekwa Uingereza kwa kifungo

Image caption Taylor alipinga hatua ya kufungwa jela Uingereza akisema ni mbali sana kwa familia yake

Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, amehamishwa kutoka jela nchini Uholanzi hadi Uingereza ambako atatumikia kifungo chake cha miaka hamsini.

Alipokea hukumu hiyo kwa tuhuma za uhalifu wa kivita nchini Sierra Leone.

Mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa ilimpata na hatia Taylor kwa kuunga mkono waasi katika nchi jirani ya Sierra Leone.

Rais huyo wa zamani alikuja baadaye kujulikana kama mkataji viungo , alijulikana kwa mauaji ya halaiki na kwa kutumia watoto kama wanajeshi.

Waasi wa Sierra Leone walimlipa kwa Almasi iliyotokana na mauaji yaliyokuwa yanafanyika nchini humo.

Bwana Taylor alitumai kuwa angehamishiwa Rwanda ambako alisema itakuwa afueni kwa familia yake kumtembelea kwani si mbali sana kama ilivyo Uingereza.

Lakini mahakama ilisema kuwa ni Uingereza pekee ambayo ilitoa hakikisho la kutekeleza kifungo cha Taylor.